About Shaaban Robert

Sheikh Shaaban bin Robert Ufukwe alizaliwa tarehe 1/1/1909 katika kijiji cha Vibambani, kusini mwa Machui, kata ya Tangasisi yapata maili sita kusini mwa mji wa Tanga katika iliyokuwa Tanganyika wakati wa ukoloni wa Wajerumani. Shaaban Robert alikuwa mtoto wa kwanza kwa baba yake, Mzee Selemani Ufukwe na wa nne kwa mama yake, Bi Mwanamwema binti Mwidau. Katika diwani yake ya Koja la Lugha, shairi la “Jina Langu Nimewapa”, Shaaban Robert anatueleza kwa muhtasari kuhusu kuzaliwa kwake, elimu, kazi na vituo alivyofanya kazi. Shaaban anasema:
NILIZALIWA Tanga, kumi na tisa na tisa
Tangu ujana natanga, kwa safari kunipasa …
Babu yake Shaaban Robert, aliyeitwa Jumaa Kanduru wa ukoo wa Chemataka alifika Dar es Salaam kutokea Tunduru akiwa na kaka yake, Abubakari. Bwana Jumaa aliajiriwa katika shamba la minazi huko Kigamboni lililokuwa linamilikiwa na mlowezi wa Kijerumani (Mdachi) ambaye inasemekana aliitwa Roberts. Baada ya kuoa, Jumaa Kanduru alijaliwa kupata mtoto wa kiume ambaye alipewa jina la Ufukwe. Inasemekana kuwa mtoto huyo alipewa jina la Ufukwe kwa sababu mama yake alipata uchungu na kujifungua akiwa ufukweni, alikokuwa amekwenda kutanda uduvi. Mtoto Ufukwe pia alipewa jina la Kiislamu, Selemani. Inasimuliwa kuwa, tajiri wa Bwana Jumaa alipopata taarifa kuwa mfanyakazi wake alikuwa amepata mtoto wa kiume, alifurahi na kusema huyo ni somo wangu, aitwe Roberts. Hivyo ndivyo jina la Robert lilivyoingia katika familia ya Kiislamu na kumfanya baba wa Shaaban awe na majina matatu, yaani Selemani Ufukwe Roberts. Jina lile likamzoea na kufanya jina la Ufukwe lisahaulike kabisa. Baada ya Ufukwe kukua na kuwa mtu mzima, alijumuika na baba yake katika kazi. Mwaka 1907 aliomba uhamisho, pengine kuepuka kufanya kazi mahali pamoja na baba yake. Ombi hili lilikubaliwa na akahamishiwa Tanga katika shamba la mkonge lililokuwa Machui - Amboni Estate. Huko aliajiriwa kama karani wa shamba.
Huko Machui, Bwana Ufukwe alikutana na kumwoa Mwanamwema binti Mwidau, wa kabila la Kimwamwende kutoka kijiji cha Msengenyeni hukohuko Machui. Bi Mwanamwema alipooana na Bwana Ufukwe, tayari alikuwa ana watoto watatu, Jaffari Kibwana, Mwinyihatibu Kibwana na Mwanagani Kibwana. Watoto hawa aliwapata kwa mumewe wa kwanza, Bwana Kibwana Jaffari. Bwana Ufukwe na Bi Mwanamwema walijaliwa kupata mtoto mmoja, Shaaban Roberts. Baada ya muda miaka kadhaa ya ndoa, wawili hawa waliachana. Hapo Bi Mwanamwema aliolewa mara ya tatu na Bwana Mwinyi Ulenge Mwarogo na kuzaa naye watoto kumi - Mwishehe Ulenge, Mwanaidi Ulenge, Mwanang’andu Ulenge, Yusuf Ulenge, Mwanahadia Ulenge, Asha Ulenge, Mwidau Ulenge, Issa Ulenge, Ali Ulenge na Maimuna Ulenge (Mulokozi, 2003). Naye Bwana Ufukwe alioa tena huko Mnyanjani na kupata watoto wawili, Mwanasaumu Roberts na Abdallah Roberts. Baadaye, alioa tena huko Saadani na kujaliwa kupata mtoto mmoja, Jumaa Roberts. Mzee Selemani Ufukwe Roberts alifariki dunia Mnyanjani tarehe 14/09/1918. (Mulokozi na Sengo, 1995; Mulokozi, 2003; Taib, 2009). Baada ya kifo cha Mzee Ufukwe, Shaaban alipelekwa Dar es Salaam kwa babu yake, Jumaa bin Kanduru.

Chimbuko, dini na kabila
Kama ilivyoelezwa awali, wazazi wa Shaaban Robert hawakuwa wa kabila moja. Wenyewe walikutana na kuoana Mkoani Tanga. Mzee Robert Ufukwe alikuwa wa ukoo wa Mganga wa kabila la Kiyao. Yeye alifika huko Tanga kama karani wa Amboni Estate akitokea Kurasini - Dar es Salaam. Mama yake alikuwa wa ukoo wa Kimwamwande, kabila la Akinangala lililokuwa mchanganyiko wa kabila ya Kizigua na Kidigo, yaani mama Uziguani na baba Udigoni. Japo alikuwa na majina mawili - moja la Kiislamu - Shaaban, na jingine la Kikristo - Robert, Shaaban Robert alikuwa Mwislamu kamili. Jina la Roberts lililotokana na umaarufu wa jina ambalo baba yake alipewa na tajiri wa Kidachi, uliokuwa na hata kuzidi lile la kikabila - Ufukwe.
Elimu: Shaaban Robert alipofikisha umri wa miaka 9, mama yake alimpeleka madrasa ili kupata elimu ya dini ya Kiislamu. Kisha, baada ya baba yake kufariki na Shaaban Robert kuhamia kwa babu yake, Dar es Salaam, alikaa kwa muda, kisha, mwaka 1922 babu yake alimpeleka Shule ya Msingi Kichwele (kwa sasa Uhuru Mchanganyiko) ambapo alijiunga Darasa la Kwanza. Mwaka 1926 Shaaban Robert alihitimu Darasa la Nne na kushika nafasi ya pili kati ya wanafunzi 11 waliofaulu mtihani wa mwisho na kupata cheti cha kumaliza shule chini ya mfumo wa elimu wa Waingereza. Katika shairi la Jina Langu Nimewapa, Shaaban Robert anazungumzia elimu yake kwa kusema:
Nilipelekwa kusoma, Dar es Salaam mjini
Nikaona taadhima, ya malezi ya chuoni …
Jina la Roberts lilipata mabadiliko ya kimatamshi na kimaandishi. Mwanzoni, akiwa shuleni, aliandika Roberts; kisha baadaye alilibadilisha kuwa Robert.

Books by Shaaban Robert

Showing 1 to 9 of 9 records (1 Pages)
Sort By:
text_showing_page_of_pages
Sort By: