Tab Article
Tamthiliya ya Morani inasawiri misukosuko ya kisiasa na kiuchumi nchini Tanzania katika miaka ya 80. Katika kiwango cha uhalisia, tunamwona Dongo, mhusika mkuu, akipambana na wahujumu uchumi ili kuwakomboa wanyonge. Lakini ghafla nyota iliyong’aa na kuwapa tumaini maskini inazima. Dongo anafariki dunia! Kwa wanyonge ukombozi wa nchi yao unageuka ndoto ya kukatisha tamaa. Kuhusu hali katika dunia ya Kuzimuni tunamwona Dongo katopea kwenye mdahalo wa kifalsafa akitafakari na kutathmini yale yaliyomfika na kumtoa roho ghafla. Katika tamthiliya hii iliyoandikwa kwa ustadi kabisa, mwandishi ameyasawiri na kuyaakisi masuala tata ya kiuchumi, kiitikadi na kihistoria mintaraf bara letu la Afrika. Hakika wapenzi wa Fasihi ya Kiswahili watapata historia, burudani na maarifa yenye kina katika tamthiliya hii.