Tab Article
Kitabu hiki kinaangazia masuala ya msingi katika safari ya elimu, kikianza na hatua ya malezi ya mtoto kabla ya kwenda shule, elimu ya awali, elimu msingi na hatimaye elimu ya sekondari. Mwandishi anaweka mkazo katika mambo ya kawaida ya kila siku ambayo yamezoeleka kuwa si ya muhimu sana, ila ambayo yana athari kubwa katika kuamua mustakabali wa maisha na mafanikio ya mtoto na jamii yake. Kusudi la kitabu hiki ni kutoa msukumo kwa wazazi, walezi, walimu na wanajamii wote kwa ujumla kutambua na kuzingatia muktadha mpana wa elimu unaohusisha malezi na maisha ya mfano ambayo, kwa pamoja yanaweza kuamua mafanikio ya mtu, jamii yake na taifa lote. Kitabu hiki kitakusaidia wewe mzazi kutambua wajibu wako katika kumpatia mwanao elimu bora. Kitakuonesha maeneo ya msingi ambayo jicho lako linapaswa kuyatazama ili kumsaidia mtoto wako na hata wa jirani yako kupata elimu sahihi na yenye tija kwake na kwa jamii yake. Pia kitabu hiki kinampatia mwalimu, mkuu wa shule na wadau wengine wa elimu namna ya kutathmini iwapo elimu anayowapatia wanafunzi ni bora au la. Mwisho, kinaikumbusha jamii inayomzunguka mtoto wajibu na umuhimu wa kumpatia malezi na mwongozo sahihi unaojumuisha nidhamu, uwajibikaji na tabia njema. Mwandishi anaiasa jamii kwa ujumla wake, kutekeleza wajibu wake wa kuwapa watu wake elimu bora. Anasema, “Jamii isiyo na wasomi bora, itachelewa kupata maendeleo na watu wake wanaweza kubaki nyuma kifikra, kimtazamo na hata kiuchumi.Jamii ya namna hii ni vigumu kufanikiwa katika ushindani na jamii au mataifa yenyewatu walioelimika.â€