Tab Article
Jaji Dr. Steven J. Bwana, kama viongozi wengi wa rika yake, alikulia kwenye mazingira duni, chini ya utawala wa wakoloni. Lakini mazingira hayo anayoeleza kwenye kitabu hiki, hayakumzuia kujiendeleza kielimu, hadi kupata shahada nne za sheria. Alipata shahada yake ya Uzamivu (PhD) mwaka 1982 katika Chuo cha Kipapa cha Laterano, Roma na hivyo. Dr. Bwana ni mmoja ya watanzania wachache wenye elimu ya juu sana kwenye fani ya sheria.
Tangu alipoapishwa kama Hakimu Mkazi, tarehe 2, Aprili 1975, hadi hapo alipostaafu kazi ya ujaji wa Mahakama ya Rufaa, tarehe 8 Januari 2015, Jaji Bwana alifanya kazi ndani na nje ya Tanzania. Aliwahi kuwa Jaji wa Mahakama Kuu na baadaye Jaji wa Mahakama ya Rufaa katika Jamhuri ya Seychelles (1994–2009). Hadi alipoandika kitabu hiki, Jaji Bwana ni Jaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Kambodia, kazi aliyoteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Jaji Bwana ameandika vitabu kadhaa; hiki ni cha kumi na mbili na hakitakuwa cha mwisho. Katika vitabu alivyoandika ni Haki, Amani na Maendeleo: Nafasi na Wajibu wa Mahakama Tanzania (Mkuki na Nyota 2008).
“Ukisoma tawasifu hii iliyoandikwa kwa ustadi sana bila majivuno yoyote, utamfahamu vizuri mzalendo huyu na mmajumui wa Afrika, mwenye kichwa chenye umahiri wa sheria uliotumikia taifa hili na mataifa mengine katika nyakati na mazingira yaliyojaa changamoto. Hapohapo utafahamu pia mchango wake katika kuifanya sheria kuwa chombo cha kuwatumikia watu wa kawaida, kwa sababu anaamini kuwa, hatima ya sheria ni kuwa nyenzo ya kutoa haki, ya kuleta amani na maendeleo.â€
—Jaji Thomas B. Mihayo