Tab Article
Tawasifu hii inafuatia wasifu wa Mwalimu Julius Nyerere na tawasifu ya Rais Benjamin Mkapa na kuziba pengo lililokuwa limebaki katika kumbukumbu ya awamu tatu za mwanzo za uongozi wa Tanzania huru.
Vitabu hivi vinasaidia kuweka historia sawa; vinaziba baadhi ya mapengo katika kuelewa mambo mbalimbali ya kihistoria. Kitabu kinaitwa “Mzee Rukhsa” kuakisi uongozi wa Rais Mwinyi aliyependa kutumia neno jepesi kama hili kuashiria mambo makubwa aliyokuwa akiyafanya kufungua mipaka ya uchumi na siasa katika Tanzania.
Mojawapo ya mambo yanayowekwa sawa humu, ni kwamba, si kweli kuwa Rais Mwinyi alimkaidi Mwalimu kwa kuanzisha mageuzi kwenye uchumi. Kwa heshima kubwa aliyokuwa nayo kwa Mwalimu, hata akajiona kama ni kichuguu mbele yake aliyemlinganisha na Mlima Kilimanjaro, asingeweza kufanya hivyo. Isitoshe, Rais Mwinyi aliongoza serikali kwa miaka mitano ya mwanzo bila kuvaa kofia ya mwenyekiti wa chama (CCM). Mwalimu asingetaka, yasingewezekana.
Mwalimu alishajaribu kila njia lakini uchumi wa Tanzania uliendelea kudorora. Hazikuwepo fedha za kigeni hata kwa mambo ya msingi kabisa. Mwalimu akampa rukhsa Mwinyi kujaribu maarifa mengine. Baadaye yalikuwapo mambo ambayo Mwalimu hakuyafurahia, akayakemea hadharani. Lakini kimsingi alikubali hoja ya mageuzi, ikiwemo kufungua uchumi kwa sekta binafsi ya ndani na nje ya nchi.
Kadhalika kwenye siasa. Mwalimu aliona umuhimu wa mageuzi kwenye siasa, ikiwemo mabadiliko yaliyoakisiwa kwenye “Maamuzi ya Zanzibar”. Kitabu kinafafanua ilivyotokea, na kwamba wazo la awali lilikuwa la Mwalimu Nyerere, ingawa baadaye kuna mambo hakuyapenda.
Kitabu pia kinazungumzia changamoto nyingi za urais wa Ali Hassan Mwinyi, ikiwemo ile ya muundo wa muungano; migomo; uzawa na chuki baina ya wafanyabiashara; migogoro ya kidini na kadhalika. Yote hayo na mengine yamewekwa vizuri katika lugha nyepesi ya kueleweka na kila mtu.
Rais Mwinyi amechukua muda mrefu kukamilisha tawasifu yake, lakini thamani yake ilitosha kusubiriwa.