Tab Article
KONGO [DRC] ilipata uhuru toka kwa Wabelgiji tarehe 30/06/1960 na Patrice Lumumba akawa Waziri Mkuu wa kwanza. Baada ya miezi sita tu, yaani tarehe 17/01/1961, Lumumba akauliwa kikatili na kinyama. Leo hii [taz.The Assassination of Lumumba - na Ludo de Witte] hakuna kaburi la Lumumba nchini Kongo kwani chini ya usimamizi wa Joseph Mobutu na Moise Tshombe, mwili wa Lumumba ulikatwakatwa vipande vipande na kutumbukizwa ndani ya pipa la tindikali na hivyo kuumaliza kabisa. Shinikizo la kutaka Lumumba afe, ima faima, lilitoka katika nchi nne: Marekani, Ubelgiji, Ufaransa na Uingireza. Kilichomponza Lumumba kuuwawa ni fikra zake za kizalendo na kimapinduzi akitaka utajiri mkubwa wa Kongo uwaendeleze Wakongo wenyewe, badala ya kuwaachia mabeberu waendelee kunyonya rasilimali za Kongo kwa faida ya nchi zao. Takribani miaka 60 imepita tangu kifo cha Lumumba lakini Kongo na Afrika bado inadaiwa kutekeleza ajenda ya Lumumba ya kuleta maendeleo ya kweli kwa mamilioni ya wananchi ambao wanaishi katika umasikini wa kupindukia. Kati ya miaka ya 1983 – 87, kwa mfano, Lumumba ‘alifufuka’ na kuishi ndani ya roho ya Thomas Sankara wa Bukina Farso; lakini Wafaransa, kwa ukatili mkubwa, hawakuchelewa kumtoa roho walipomwona anakazania kuikata minyororo ya uchumi tegemezi toka kwa Wafaransa na mabeberu kwa ujumla. Safari ni ndefu na vita ni vikali, lakini tutashinda, hatimae! Viva Afrika! Viva!
Tamthilia hii inasisimua, inahuzunisha na inadokeza masuala muhimu ya kihistoria, kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni mintaarafu Bara letu la Afrika.